11 Februari 2023 - 20:33
Mshauri wa Bashar Assad: Vikwazo vya Magharibi vinatatiza utoaji wa misaada kwa waathiriwa wa tetemeko la ardhi

Mshauri wa vyombo vya habari wa Rais wa Syria amesema: Kinachozidisha hali mbaya ya sasa kwa watu waliokumbwa na janga la tetemeko la ardhi ni vikwazo vya Marekani na Ulaya dhidi ya Syria.

Bouthaina Shaaban, mshauri wa vyombo vya habari wa Rais wa Syria amesema kinachofanya hali ya sasa kuwa mbaya zaidi ni vikwazo vya Marekani na nchi za Ulaya dhidi ya Syria, ambavyo vinazuia kusasisha zana na mbinu za kufikisha misaada kwa waathiriwa wa tetemeko la ardhi.

Ameashiria ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na Marekani dhidi ya watu wa Syria na kuongeza kuwa: Nchi za Magharibi daima zimekuwa zikiyapa kipaumbele masuala ya kisiasa badala ya masuala ya kibinadamu.

Ijapokuwa baadhi ya nchi kama vile Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zinaendelea kutuma misaada ya kibinadamu katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi nchini Syria lakini wakati huo huo vikwazo vya nchi za Magharibi hususan Marekani, vinatatiza operesheni za kufikisha misaada hiyo katika baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko la ardhi nchini Syria, na ndege nyingi za kubeba misaada kwa wahanga wa tetemeko la ardhi zimeshindwa kuingia Syria kutokana na vikwazo hivyo.

Juzi Alkhamis Rais Bashar al-Assad wa Syria alifichua kuwa Marekani inatoa mashinikizo kwa nchi zinazotaka kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi nchini Syria. 

Tetemeko la ardhi la ukubwa wa 7.8 katika kipimo cha Rishta lilitikisa kusini mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria Jumatatu asubuhi ya tarehe 6 Februari na hadi sasa limesababisha vifo vya zaidi watu elfu 23 katika nchi hizo mbili. 

342/